Skip to main content

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - FASIHI KWA UJUMLA

 
  FASIHI KWA UJUMLA
 

Fasihi ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayomhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake. (Wamitila, 2004). Fasili hii imejaribu kufafanua vizuri kile ambacho fasihi inajihusisha nacho, kimsingi fasihi inajihusisha na wanadamu. Vitu vya msingi tunavyoviona katika fasili hii ni kwamba fasihi ni sanaa, na fasihi inatumia lugha lakini zaidi fasihi inajihusisha na wanadamu.

Dhima za Fasihi katika Jamii

Dhima za fasihi katika jamii ni pamoja na hizi zifuatazo:

1. Kuburudisha jamii:Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.

2. Kuelimisha. Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mabalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.

3. Kuonya jamii. Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.

4. Kuunganisha jamii. Fasihi huleta watu katika jamii. Watu huunganishwa kupitia kazi mbalimbali za kifasihi, kwa mfano, kupitia nyimbo, miviga, vichekesho na kadhalika.

5. Kukuza lugha.Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.

6. Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.

7. Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.

                              
                 AINA ZA FASIHI

Kuna tanzu mbili za fasihi, ambazo ni fasihi andishi na fasihi simulizi.

1. FASIHI SIMULIZI

Fasihi Simulizi ni utanzu wa fasihi ambao unawakilisha sanaa ya lugha inayopitishwa kutoka kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno/masimulizi ya mdomo.

Sifa za Fasihi Simulizi

1. Hupitishwa kwa njia ya mdomo

2. Ufanisi wa sanaa katika fasihi simulizi hutegemea uwezo wa msimulizi, au wahusika.

3. Masimulizi yake yanaweza kuathiriwa na mazingira, hisia na hali

4. Ni mali ya jamii. Hakuna mtu fulani anayemiliki sanaa katika fasihi simulizi.

5. Inaweza kubadilika kutoka kizazi hadi kizazi, au mazingira mbalimbali kwa sababu hutegemea kumbukumbu ya msimulizi.

6. Aghalabu huwa na funzo fulani

Dhima za Fasihi Simulizi

1. Kuburudisha - Hufurahisha na kuchangamsha hadhira

2. Kunasihi - kutolea mawaidha na kuonyesha mwelekeo unaotarajiwa katika jamii.

3. Kuelimisha watu kuhusu vitu mbalimbali hasa mazingira yao

4. Kutambulisha jamii - jamii mbalimbali husifika kutokana na sanaa zao katika fasihi simulizi kama vile nyimbo.

5. Kuhifadhi na kudumisha utamaduni wa jamii

6. Kuunganisha watu - huleta watu pamoja

7. Kukuza lugha - fasihi huimarisha lugha kwa kuwa hutumia mbinu mbalimbali za lugha.

8. Kuliwaza - hutoa huzuni na kuleta matumaini.

9. Kupitisha muda - wakati mwingine fasihi simulizi hutumika kupitisha muda.

10. Fasihi simulizi ni chombo cha mawasiliano hususani kupitia ngomezi.


2. FASIHI ANDISHI

Fasihi Andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno ya maandishi kupitisha ujumbe kwa hadhira.

Kuna tanzu kuu nne za Fasihi Andishi:

1. Hadithi Fupi – Hii ni kazi ya fasihi andishi yenye kisa kimoja na mhusika mkuu mmoja na maudhui yake sio changamani.

2. Riwaya –Ni kazi ya fasihi andishi yenye wahusika wengi na muundo changamani ni ndefu na maudhui yake ni mapana.

3. Tamthilia- ni kazi ya kisanaa yenye muundo wa kiugizikaji inayowasilishwa katika maandishi.

4. Mashairi - mashairi yakiwa yamechapishwa pia hutambulika kama fasihi andishi.
            

Sifa za Fasihi Andishi
1. Hupitishwa kwa njia ya maandishi
2. Ni mali ya mtu binafsi
3. Haiwezi kubadilishwa papo kwa papo
4. Hutumia mbinu za lugha na mbinu za sanaa katika uwasilishaji wake.

Dhima za Fasihi Andishi
1. Kukuza lugha
2. Kuhifadhi kazi ya sanaa katika maandishi
3. Kuburudisha
4. Kuelimisha
5. Kukashifu tabia zisizoandamana na maadili ya jamii
6. Kuonya, kuelekeza, kunasihi

Tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi

Zifuatazo ni tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi kama zilivyobainishwa katika jedwali hapa chini: 


Popular posts from this blog

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - UANDISHI WA BARUA

   UANDISHI WA BARUA     Uandishi Wa Barua   Barua za kirafiki ambazo pia huitwa za kidugu huandikwa baina ya watu wa undugu au jamii moja. Katika mada hii utaweza kujifunza muundo wa uandishi wa barua ya kirafiki na jinsi ya kuandika barua ya kirafiki. Utaweza kutofautisha kati ya barua ya kirafiki na ile isiyokuwa ya kirafiki.   BARUA ZA KIRAFIKI   Iwapo ni katika ndugu barua za kirafiki zaweza kuwa kwa watu kama: baba, mama, shangazi, mume, mke, mtoto, na kadhalika. Katika jamii waandikiwao barua za kirafiki ni kama jirani, rafiki, mpenzi, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mgonjwa, na kadhalika.   Muundo wa Barua za Kirafiki   Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa barua za kirafiki:   1. ANWANI kamili ya mwandishi, katika herufi hukaa juu upande wa kulia mwa karatasi.   2. TAREHE, chini ya anwani.   3. MTAJO wa heshima kwa anayeandikiwa, kama vile, mpendwa, mpenzi, na kadhalika, huan...

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - USIMULIZI

  USIMULIZI Usimulizi ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani. Katika mada hii utajifunza juu ya taratibu za usimulizi wa matukio kupitia njia kuu mbili za masimulizi, yaani kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Pia utaweza kujifunza juu ya mbinu mbalimbali za usimulizi.   USIMULIZI WA HADITHI   Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua. Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana. USIMULIZI WA HABARI   Taratibu za Usimulizi wa Matukio: Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumwe...

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - UFAHAMU

  UFAHAMU Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.   KUSIKILIZA   Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.   Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusikiliza   Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:   1. Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa   2. Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza   3. Kuelewa sintaksia (muundo wa m...

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - AINA ZA MANENO

AINA ZA MANENO Katika lugha ya Kiswahili kuna angalau aina nane za maneno ambazo wataalamu wengi wa lugha wanakubaliana hivyo. Katika mada hii utaweza kujifunza na kubainisha aina zote nane za maneno na jinsi zinvyotumika katika sentensi. Utaweza pia kujifunza namna ya kutofautisha aina za maneno ambazo zimeleta ubishi miongoni mwa wataalamu wengi hususani katika Viunganishi na Vihusishi.   Aina Saba za Maneno ya Kiswahili                                             Aina za maneno katika lugha ya Kiswahili ni pamoja na hizi zifuatazo:   Aina Nomino (N)                                                                   ...

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - FASIHI SIMULIZI

  FASIHI SIMULIZI   Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu.   Tanzu za Fasihi Simulizi   Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.   Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: - Masimulizi/hadithi  - Semi - Ushairi - Mazungumzo - Maigizo  - Ngomezi   Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi   1.  SIMULIZI/ HADITHI   Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahili. Urefu wa hadithi hutofautiana k...

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA - MAWASILIANO

MAWASILIANO Katika mada hii unatarajiwa kuelewa fasili ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha fasili ya lugha. Utaelewa dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Lugha kama Chombo cha Mawasiliano Mawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia, malengo, tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni binadamu). Maana ya Mawasiliano Lugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza kwamba mwasiliano yangekuwaje pasipokuwepo lugha? Mwalimu angekua anatumia mt...