UANDISHI WA BARUA
Uandishi Wa Barua
Barua za kirafiki ambazo pia huitwa za kidugu huandikwa baina ya watu wa undugu au jamii moja. Katika mada hii utaweza kujifunza muundo wa uandishi wa barua ya kirafiki na jinsi ya kuandika barua ya kirafiki. Utaweza kutofautisha kati ya barua ya kirafiki na ile isiyokuwa ya kirafiki.
BARUA ZA KIRAFIKI
Iwapo ni katika ndugu barua za kirafiki zaweza kuwa kwa watu kama: baba, mama, shangazi, mume, mke, mtoto, na kadhalika. Katika jamii waandikiwao barua za kirafiki ni kama jirani, rafiki, mpenzi, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mgonjwa, na kadhalika.
Muundo wa Barua za Kirafiki
Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa barua za kirafiki:
1. ANWANI kamili ya mwandishi, katika herufi hukaa juu upande wa kulia mwa karatasi.
2. TAREHE, chini ya anwani.
3. MTAJO wa heshima kwa anayeandikiwa, kama vile, mpendwa, mpenzi, na kadhalika, huandikwa kushoto, baada ya tarehe.
4. UTANGULIZI wa barua yenyewe ambao kwa desturi huwa ni salamu.
5. BARUA YENYEWE ambayo ndiyo kiini cha waraka.
6. SALAMU za kumalizia, pengine kwa jamaa na jamii.
7. HITIMISHO, katika aya, maalumu ambayo huwa, kwa mfano: ‘Ni mimi baba yako akupendaye, na kadhalika.
8. SAHIHI ambayo si sharti wala muhimu sana.
9. JINA au MAJINA ya mwandishi, mwishoni.
Tazama mfano wa barua ya kirafiki:
Mfano 1
MUSOMA FISH PACK
S.L.P 4546
MUSOMA
23/5/2013
Mwanangu Nyamchele,
Ninafuraha kukujulisha kuwa nimepokea barua yako. Mambo yote uliyoyaeleza nimeyaelewa barabara. Huku nyumbani sote tu wazima na ni matumaini yetu kwamba afya yako ni nzuri.
Tabia ya kulalamikia chakula ni mbaya. Tabia kama hii ikikomaa husababisha ulafi. Kumbuka hukwenda shuleni kula kama nguruwe. Huko shuleni nimekupeleka ili usome kwa bidii na ujifunze mengi. Usitamani kustarehe na kufikiria maakuli na anasa zingine za ulimwengu huu. Ondoa fikira za chakula akilini mwako na uache uzembe, eboo!
Hebu nikuonye kuhusu kuwapima na kuwachagua walimu. Walimu katika shule hiyo ni wabobezi na ndio maana nikakupeleka hapo. Wanajua mnayostahili kufundishwa. Huna ruhusa ya kusema eti walimu wengine ni wakali na hufundisha haraka haraka sana. Wewe unahitaji kutega sikio na kutii. Ukiwa makini na uwe na imani utayaelewa mambo unayofundishwa. Usisahau kuwa mchagua jembe si mkulima.
Mambo makubwa unayostahili kuyatilia bidii ni masomo yako. Muda wa miaka minne ni mfupi sana. Uonyeshe adabu njema kila wakati. Uwaonyeshe walimu wako taadhima na uwatii daima dawamu.
Jambo lililo kubwa katika shughuli yoyote ni uvumilivu. Ukivumilia utavuna matunda mabivu. Sitachoka kukusisitizia, ‘Ukilima pantosha, utavuna pankwisha.’ Fanya kila jitihada utimize mambo mengi iwezekanavyo kuanzia leo lakini usipapie chochote. Ndo ndo ndo hujaza ndoo.
Mungu akubariki. Umwombe akusaidie katika kila jambo. Ujiepushe na maovu yoyote yale. Ukiwa na jambo usiwe na hofu kutuarifu mara moja. Mama yako amekusalimu sana. Amenikumbusha nikupashe hakuna refu lisilo na ncha.
Kwaheri kwa sasa.
Ni mimi, baba yako akupendaye,
Magafu Malima